16 Sep 2019 Toleo la habari Mabadiliko ya tabia nchi

Profesa Katharine Hayhoe kutoka Kanada ndiye mshindi wa Tuzo la Bingwa wa Dunia lilnalotolewa na Umoja wa Mataifa

  • Raia wa Kanada, mwanasayansi wa masuala ya hali ya hewa, Profesa Katharine Hayhoe ndiye mshindi wa Tuzo la Bingwa wa Dunia lilnalotolewa na Umoja wa Mataifa, katika kitengo cha sayansi na ubunifu.
  • Ametuzwa kutokana na ujuzi wake na kwa kupenda kuangazia masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

 

 

Septemba 16,  2019 --Raia wa Kanada, mwanasayansi wa masuala ya hali ya anga, Profesa Katharine Hayhoe ndiye mshindi wa Tuzo la Bingwa wa Dunia mwaka wa 2019. Amepokea tuzo la kiwango cha juu sana linalotolewa na Umoja wa Mataifa kutokana na juhudi zake za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na juhudi zake za kipekee za kusaidia kubadilisha mielekeo ya watu. 

 

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lilimtuza Hayhoe katika kitengo cha sayansi na ubunifu.

 

Hayhoe ni profesa katika Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Texas Tech na nimkurugenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa. Utafiti wake umekuwa na manufaa kwa uundaji wa sera Marekani katika majimbo na katika serikali za mitaa nchini Marekani na kwengineko. 

 

Pia, ni mmojawapo wa washawishi wakubwa duniani wanaozungumzia hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi na anaheshimiwa mno kutokana na uwezo wake wa kuelimisha watu zaidi kuhusu wanayafahamu na kuwaonyesha madhara watakayokumbana nayo kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

 

Hayhoe ni mwandishi mkuu wa ripoti nyingi muhimu zinazohusu mazingira, ikiwa ni pamoja na ripoti ya Marekani ya ‘US Global Change Research Program’s Second, Third, and Fourth National Climate Assessments'. Pia, amefanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika miji na kanda na kuwawezesha wadau kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa chakula, maji na miundo mbinu na kuonyesha umuhimu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya kitaifa na kikanda.

 

"Profesa Katharine Hayhoe amejitolea maishani mwake kufanya utafiti kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na kueneza matokeo ya tafiti zake mbali iwezekanavyo ili kuchochea waunda sera na wananchi kuchukua hatua,"  alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.

 

"Tunapoongeza juhudi zetu mara dufu ili kupunguza athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji watu wa kujitolea sana, wanaosababisha mabadiliko kutokana na elimu walio nayo watuongoze jinsi tunavyoweza kuwa na siku zijazo endelevu. Kwa kuwa mtaalamu asiyechoka, Profesa  Hayhoe anatuongoza huku tukimfuata." Andersen alisema.

 

Wakati wa Mkutano Mkuu wa Kushughulikia Mazingira wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika tahere 23 Septemba katika mji wa New York, Suala la umuhimu wa kuchukua hatua kali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi litaangaziwa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa viongozi duniani, wamiliki wa biashara na mashirika ya uraia kuhudhuria mkutano wakiwa na suluhisho jinsi watakavyopunguza uchafuzi wa hewa kwa asilimia 45 kufikia karne ijayo na kuepukana na hewa chafu kabisa kufikia mwaka wa 2050. Hii ni sambamba na Makubaliano ya Paris kuhusu  tabianchi na Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

 

Hayhoe, ambaye ni mke wa mchungaji ambaye pia huandika vitabu Andrew Farley, ni mshindi wa matuzo kadhaa kutokana na kazi yake. Mojawapo ya matuzo hayo ni Tuzo la nane la 'Stephen H. Schneider Award for Outstanding Climate Science Communication' katika mwaka wa 2018. Pia, alitambuliwa na gazeti la TIME's kam mmojawapo wa watu waliokuwa na ushawishi mkubwa katika mwaka wa 2014. Pia alitambuliwa mara pili kama 'Foreign Policy’s 100 Global Thinkers', mwaka wa 2014 na mwaka wa 2019.

 

"Nina furaha isiyokuwa na kifani kutuzwa na Umoja wa Mataifa," alisema Hayhoe, ambaye pia alitambuliwa na FORTUNE kama mmojawapo wa viongozi 50 waliojitolea zaidi. Pia alipokea tuzo la ‘Sierra Club’s Distinguished Service award’. 

 

"Tuzo hili linatutia moyo wa kuendelea kufanya kazi yetu ya kila siku ya kusambaza ujumbe kuhusu uhalisia wa mabadiliko ya tabianchi na tunapaswa kuchukua hatua za kukuabiliana nayo. Tukishirikiana, licha ya shinikisho, tutafaulu kwa sababu tayari tuna teknolojia na maarifa ya kuleta mabadiliko yanayohitajika. Kinachokosekana tu ni kujitolea,"alisema Hayhoe.

Mabingwa wa Dunia, ni tuzo la kimataifa linalotolewa na Umoja wa Maataifa kwa heshima ya mazingira. Lilianzishwa na UNEP mwaka wa 2005 kuwatuza watu wa kipekee ambao matendo yao yamekuwa na athari chanya zinazoleta mabadiliko kwa mazingira. Kutoka kwa viongozi duniani hadi kwa watetezi wa mazingira na hadi kwa wanaobuni teknolojia, waanzilishi hawa wanaleta mabadiliko ili kutunza sayari yetu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

 

Hayhoe ni mmoja wa washindi wa huu mwaka. Vitengo vingine ni pamoja na Uongozi wa sera , motisha na kuchukua hatua  na sayansi na ubunifu  Washindi wa mwaka wa 2019 watatuzwa wakati wa sherehe ya gala mjini New York tarehe 26 Septemba wakati wa kikao cha 74 cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Wengine watakaotuzwa pia wakati wa tukio hili ni wanamazingira wa kipekee saba wa umri wa kati ya miaka 18 hadi miaka 30. Watatuzwa tuzo la Vijana Bingwa Duniani. 

 

Watu waliowahi kushinda tuzo la Mabingwa wa Dunia katika kitengo cha sayansi na na ubunifu ni pamoja na Impossible Foods na Beyond Meat katika mwaka wa 2018 kwa kutengeneza baga mbadala badala ya baga za nyama; Mwanamtindo kutoka Australia Leyla Acaroglu ni mshindi wa mwaka wa 2016 kwa kazi yake endelevu; na mwanakemia wa masuala ya anga Sir Robert Watson ni mshindi wa mwaka wa 2014.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

UNEP ni msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

 

Kuhusu Weibo

Mabingwa wa Dunia huandaliwa kwa msaada wa ufadhili kutoka kwa Weibo-Mtandao mkuu wa kijamii nchini China unaowezesha watu kuunda, kushiriki na kupata makala mtandaoni. Weibo ina zaidi ya watumizi 486 kila mwezi. www.weibo.com

 

Kuhusu Mabingwa wa Dunia

Tuzo linalotelewa kila mwaka la Mabingwa wa Dunia, hutuza viongozi vya kipekee kutoka kwa serikali, mashirika ya uraia na sekta ya kibinafsi ambao matendo yao yamesababisha mabadiliko chanya kwa mazingira. Tangu mwaka wa 2005, tuzo la Mabingwa wa Dunia limewatuza washindi 88, kuanzia kwa wakuu wa nchi hadi kwa wanaobuni teknolojia .  Tembelea tovuti.

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keisha Rukikaire, UNEP News & Media, [email protected], +254 722 677747