19 Jul 2019 Tukio Nature Action

Mwito wa mwisho wa kuleta mabadiliko kwa mifumo ya chakula

Nusu ya idadi ya watu duniani hushiriki moja kwa moja katika kilimo na takribani asilimia 40 ya ardhi hutumiwa kukuza mimea na kufuga wanyama. Uzalishaji wa chakula hutuwezesha sisi sote kuwa hai na hupatikana kwa gharama pia: vyanzo vya maji viko karibu kuangamia na huchafuliwa kutokana na uzalishaji wa chakula. Pia, ulaji wa chakula kinachoathiri afya unawekea taasisi za matibabu shinikisho.

Licha ya changamoto kubwa zinazokabili sekta ya kilimo, uzalishaji wa chakula pia unatoa fursa kubwa ya kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na malengo ya mkataba wa Paris wa Tabia Nchi huku ukikabiliana na uaribifu wa mazingira na uangamiaji wa bayoanwai. Ila, ni sharti tubadili jinsi tunavyojilisha. Na tunapaswa kufanya hivyo upesi.

"Ifikiapo mwaka wa 2050, sayari yetu itahitaji kulisha watu wapatao bilioni 10. Ni muhimu kufanyia mabadiliko mifumo ya kilimo na mzunguko wa chakula ili ifanye kazi kwa ushirikiano na mazingira bali siyo kukabiliana nayo. Hii ndiyo njia ya pekee ya kuhakikisha watu kila mahali wanapata lishe bora lenye virutubishi," asema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.  

Mnamo Aprili mwaka wa 2018, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa pamoja na wabia wengine wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, lilizindua mradi mpya wa kukabiliana na masuala haya.

Mradi wa Kuimarisha Ekolojia kupitia Kilimo (Scaling Up Agroecology) una nia ya kuonyesha jinsi mifumo anwai ya kilimo kinachotilia maanani ekolojia ni muhimu siyo tu katika kukabiliana na umaskini, njaa na mabadiliko yantabia nchi na jinsi ya kuyarebisha, lakini pia uwezesha kufikia Malengo 12 kati ya 17 ya Maendeleo Endelevu katika nyanja kama vile za afya, elimu, jinsia, maji, nishati na ukuzaji wa uchumi.

image
Ploti ya kufanyia majaribio ya uzalishaji wa kiasili wa mtama wa aina ya proso na mchicha kule Humla, Nepal, mojawapo wa mradi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa/Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira  "Kujumuisha Mimea ya Kiasili yenye jeni anwai katika Teknolojia: Kutumia Mbinu ya  Vitu Mbalimbali vya Bayoanwai ili Kupunguza athari za Mabadiliko Yasiyotabarika ya Tabia Nchi kwa Mazingira katika eneo la Nepal Himalayas”. Picha na Saroj Pant, Miradi ya Kiasili ya Bayoanwai, Utafiti na Maendeleo.

Agroekolojia ni matumizi ya dhana za kiekolojia na kijamii pamoja na kuwa na msimamo katika mifumo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo. Hakuna kijelezi kimoja, lakini inaashiria kutunza ardhi kwa njia endelevu, inayojumuisha  mifumo anwai ya uzalishaji, ikiwa ni pamoja na kufanya kilimo ndani ya misitu. Ina uhusiano wa karibu na kilimo kisichotumia kemikali au kilimo kisichokuwa cha gharama ya juu. Istilahi zingine kama vile kilimo cha mimea inayootesha mara kadhaa au kilimo cha kiekolojia pia hutumika.

"Agroekolojia hupatikana katika maandishi ya kisayansi tangu miaka ya 1920, na hutumiwa na wakulima katika jamii. Pia hutumiwa nyanjani na mashirika yanapigania kuwepo kwa uendelevu katika jamii  na pia kwenye sera ya umma za nchi kadhaa kote ulimwenguni," anasema Emma Siliprandi, msemaji mkuu wa Mradi wa Kuimarisha Ekolojia kupitia Kilimo katika Shirika la Kilimo na Chakula.

Kupata Umaarufu

Kufikia mwaka wa 2013, Shirika la Kilimo na Chakula halikutilia maanani zaidi agroekolojia. Lakini mambo yamebadilika sana tangu hapo, huku serikali na wakulima kote ulimwenguni wakigundua kuwa kuweka dawa ya kuua wadudu na mbolea nyingi kwenye mimea haihitajiki, haijitoshelezi au, kwa kipindi cha mda mrefu, haina faida.

“Agroekolojia ni kutilia maanani bayoanwai katika kilimo na kupunguza mwanya uliopo kati ya wazalishaji wa chakula na watumizi wake," asema Emile Frison, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bayoanwai ya Kimataifa, mpiganiaji mkubwa wa masuala ya agroekolojia, na mwanachama wa sasa wa Jopo la Wataalamu wa Kimataifa wa Mifumo Endelevu ya Chakula (IPES-Food).

image
Wakulima katika eneo la Soliobod, Uzbekistan, wanapokea mafunzo ya jinsi ya kupanda miche ya kiwango cha juu ya matunda ya kiasili, chini ya mradi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa/Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira  "Kuhifadhi na Kutumia Bayoanwai ya Kilimo ili Kuboresha, Kudhibiti na Kukuza Huduma za Mfumo wa Ikolojia katika Uzalishaji wa Kilimo". Picha na Shuhrat Ahmedov

"Inahusu kuepukana na ukuzaji wa mmea mmoja na kufanya kilimo cha mimea anwai. Inahusu kuacha kupigia upatu mazao mengi na kusisitiza mno kuhusu umuhimu wa afya duniani na manufaa kwa mazingira na pia kudumisha upatikanaji wa kipato na utunzaji wa mchanga mwaka mzima na ukuzaji wa aina mbalimbali ya mimea ya kiasili. Inahusu masoko ya wakulima. Inahusu utunzaji wa vichavushaji vinavyodidimia tunavyovitegemea kupata aina nyingi ya chakula tunachokula. Inahusu kupanda tena miti na ua ili kusaidia ndege na wanyama pori wengineo," anasema.

Siliprandi anasema kuwa agroekolojia "inaanzia kutoka kwa ngazi ya chini hadi ya juu na inategemea na maeneo hali inayopelekea kupata suluhisho kwa matatizo ya wanakijiji kwa kuzingatia muktadha".

"Uvumbuzi wa kiagroekolojia hutegemea kubuni maarifa mapya, kwa kutumia sayansi na njia za kiasili, kupitia kwa desturi na maarifa ya kiasili ya wazalishaji. Kupitia uboreshaji na kuimarisha uwezo wao, agroekolojia huwawezesha wazalishaji na wanajamii kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko," anaongezea.

Kinyume na imani iliopo, pia inasaidia kukabiliana na njaa. Kuwepo kwa zaidi ya watu milioni 800 wasiopata lishe bora duniani—idadi inayoendelea kuongezeka na wala haipungui—na kuwepo kwa janga la kimataifa la watu wenye unene kupindukia, agroekolojia inaweza, na inatoa masuluhisho mapya.

Chukulia Andhra Pradesh nchini India. Serikali inaendeleza agroekolojia kwa kiwango kikubwa, na inafaulu. Wakulima zaidi wanajiunga na mradi.

Kupunguza kwa bayoanuai katika kilimo, mifumo ya chakula na lishe

Katika miaka 100 iliyopita, zaidi ya asili mia 90 ya aina ya mimea imetoweka kwenye mashamba ya wakulima. Nusu ya aina ya wanyama wengi wanaofugwa nyumbani wameangamia, na maeneo 17 makuu ya uvuvi yanafuliwa samaki zaidi kuliko uwezo wake. Hali hii nasababisha madhara kwa mazingira na ina madhara ya kiafya.

image
Picha na Flickr

"Mifumo ya uzalishaji wa aina mbalimbali ya vyakula vya kiasili, ambavyo vinastahimili mabadiliko ya tabia nchi, imo hatarini," anasema Marieta Sakalian, mtaalamu wa bayoanwai wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa. "Kutobadilisha aina ya vyakula ina uhusiano wa moja kwa moja na athari za kiafya, kwa mfano kisukari, unene kupindukia, utapiamlo, na pia huathiri upatikanaji wa dawa ya kienyeji.

"Ukuzaji na utumiaji wa mbinu za ukulima za kiekolojia unapaswa kuongezeka ili kurutubisha mchanga, kupunguza matumizi ya kemikali, kupunguza uchafuzi na kuimarisha kilimo," Sakalian anaongezea.

Ili kuleta mabadiliko, elimu ina nafasi kubwa. "Watoto wanapaswa kufundishwa kuhusu agroekolojia wakiwa chekechea," asema Frison.

Kazi ya Jopo la Kimataifa la Wataalamu kuhusu Mifumo Endelevu ya Chakula hulenga kukuza mifumo endelevu ya chakula inayofanya kazi kwa kuzingatia vipengele vya mazingira, afya, jamii, utamaduni na uchumi. Mtindo ulio na mpangilio maalum na unaokata katika nyanja mbalimbali unahitajika ili kutambua umuhimu wa elimu jaribati ya jadi na ya kiasili. Pia mbinu inayozingatia uchumi na siasa inayotambua umuhimu ma matumizi mazuri ya mamlaka na athari zinatokana na wahusika katika mfumo wa chakula ni muhimu.

Azimio la Mkutano Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi wa Machi mwaka wa 2019 kwa anwani ya Innovation on biodiversity and land degradation, “linahimiza Nchi Wanachama kuimarisha kujitolea kwao na kuongeza juhudi zao za kukomesha udidimiaji wa bayoanwai ya kibayolojia na uharibifu wa ardhi na mchanga.”

Kazi Muhimu za Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa.

image

Mkutano wa UN Climate Action Summit utafanyika Mjini New York tarehe 23 Septemba mwaka wa 2019 ili kuimarisha na kuongeza utenda kazi juu ya udharura wa kushughulikia tabia nchi duniani na kuwezesha utekelezaji kwa kasi wa Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya tabia nchi. Mwenyeji wa Mkutano wa 2019 wa UN Climate Action Summit ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Marieta Sakalian