Shirika la Andalou kupitia AFP/Minasse Wondimu Hailu
04 Sep 2023 Tukio Usafiri

Majiji barani Afrika yanakumbatia kutembea na kuendesha baiskeli huku janga la mabadiliko ya tabianchi likizidi kuwa baya zaidi

Shirika la Andalou kupitia AFP/Minasse Wondimu Hailu

Kila asubuhi mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia wenye shughuli nyingi, hali ni ile ile.

Jua linapochomoza, maelfu ya wasafiri husongamana kutafuta nafasi kwenye mabasi madogo ya umma. Wengine hukimbilia foleni ya reli jijini, mtandao wa kwanza wa kipekee barani Afrika. Baiskeli zinaonekana kutokuwepo; waendesha baiskeli si kitu kinachoshuhudiwa kila mara kwenye barabara kuu zilizopo.

Ephrem Bekele Woldeyesus anataka kubadilisha hali hii. Mtu huyu mwenye umri wa miaka 34 alianzisha na mwenzake shirika la jamii linalojulikana kama, Along the Way, linalolenga kufanya uendeshaji wa baiskeli kuwa jambo la kawaida katika mji mkuu, kwa sehemu fulani kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa unayochangia janga la mabadiliko ya tabianchi.

"Ni nzuri kwa mazingira na afya ya watu," Woldeyesus alisema kuhusu uendeshaji wa baiskeli. "Lakini hapa, watu wanafikiri sio salama. Kuna magari mengi sana.” 

Woldeyesus ni miongoni mwa idadi inayoongezeka ya wahamasishaji na maafisa wa serikali wanaotaka kufanya uendesahaji wa baiskeli na kutembea kuwa salama katika miji ya Afrika, ambako barabara huwa hatari sana. Wanaamini kuwa hiyo itasababisha watu wengi zaidi kuchagua kile kinachojulikana kama safari mazoezi, kupunguza hewa ya ukaa na kusaidia kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi ambalo tayari ni hatari katika bara lililo na watu bilioni 1.3. 

"Kutembea na kuendesha baiskeli kuna manufaa mengi kwa watu na sayari, huboresha afya, hupunguza kiwango cha gesi ya ukaa tunachozalisha na kuboresha hewa." 

Rob de Jong, UNEP

Kwenye ajenda

Usafiri mijini utaangaziwa katika Wiki ya Tabianchi barani Afrika mwaka wa 2023, itakayofanyika kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 8 Septemba jijini Nairobi, Kenya. Hafla hiyo ya kila mwaka, ambayo itashirikisha watungasera kutoka barani kote, inaendeshwa ili kusaidia mataifa ya Afrika kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na kupunguza uzalishaji wake wa gesi ya ukaa. Kanda hii, hata hivyo, ni wachangiaji mojawapo ya wadogo zaidi wa mabadiliko ya tabianchi.

Kwa njia nyingi, Ethiopia imekuwa kielelezo kwa uwezo wa kushughulikia mazingira kupitia usafiri mazoezi. Nchi hiyo, kwa ushirikiano na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), imezindua jitihada kabambe za kuwashawishi wananchi kuendelea kutembea na kuendesha baiskeli huku wakiepuka magari yanayotoa moshi mwingi.

People walking on the street
Nchi kama Rwanda zinajitahidi kufanya barabara zake kuwa salama zaidi, na kutoa msururu wa hatua za kuwalinda wanaotembea na waendesha baiskeli. Picha: Shirika la Andalou kupitia AFP/Cyril Ndegeya

Kiini cha msukumo huo ni Mkakati wa Usafiri Bila Magari. Mkakati uliozinduliwa katika mwaka wa 2020, unaweka malengo kadhaa ya miaka 10, ikijumuisha ujenzi wa kilomita 3 za njia za wanaotembea na kilomita 2 za njia za baiskeli kwa kila watu 10,000. Pia inalenga kuweka idadi ya kilomita zinazosafiriwa na magari ya kibinafsi hadi viwango vya 2020 na kupunguza vifo vya watembeaji na waendesha baiskeli kwa asilimia 80 chini ya viwango vya mwaka wa 2019. 

Hilo linachukuliwa kuwa swala muhimu la kuhimiza watu kutumia baiskeli.

Nchini Ethiopia, kuna takriban vifo 27 vya barabarani kwa kila watu 100,000 kwa mwaka, kwa mjibu wa Shirika la Afya Duniani Idadi ya vifo inachukuliwa kuwa kubwa ikizingatiwa kuwa kuna magari milioni 1.1 tu kwa idadi ya watu milioni 99.

Mbali na mkakati wa usafari mazoezi, Ethiopia pia imezindua mipango ya usalama barabarani na usafiri huku ikianzisha ushirikiano na sekta ya kibinafsi ili kuboresha miundomsingi ya kutembea na kuendesha baiskeli.

"Kuendesha baiskeli kuna manufaa kwa sababu kunajali mazingira, ni nafuu na kuna manufaa ya kiafya," alisema Fetiya Dedegeba, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Usalama Barabarani na wa Bima nchini Ethiopia.  

Vuguvugu la Afrika nzima

Vuguvugula la usafari mazoezi linaenea kote barani Afrika. Jijini Nairobi, barabara zote mpya zimejengwa kwa kutenga njia ya watembeaji na waendeshaji wa baiskeli. Asilimia 20 ya bajeti ya usafiri jijini Nairobi imetengewa usafari mazoezi, sera ambayo UNEP imesaidia kuipigania. 

Rwanda imeanzisha siku baada ya wiki mbili za kutotumia magari ambapo barabara zinageuzwa kutumiwa na wanaotembea, wakimbiaji wa mazoezi ya viungo, michezo ya kuteleza na waendesha baiskeli. Guraride, apu inayoruhusu watumiaji kukodisha baiskeli na magurudumu mawili yanayotumia umeme, pia imeanzishwa.

Vilevile, nchi hiyo, kwa usaidizi wa UNEP, iliunda sera ya kitaifa ya usafiri inayotaka barabara zote mpya kujengwa kwa njia za kupunguza foleni na kuwa na njia za kutosha, na kuzifanya kuwa salama zaidi kwa waendesha baiskeli na watembeaji. 

Hata hivyo, kote barani Afrika, barabara bado ni hatari. Bara hili hushuhudia asilimia 20 ya vifo vya barabarani kote duniani, licha ya kuwa na asilimia 3 tu ya magari yaliyosajiliwa duniani. Wastani ya watu 260 wanaotembea na waendesha baiskeli 18 huuawa barani Afrika kila siku. Hiyo inachangiwa zaidi na ukosefu wa miundomsingi, mpangilio mbaya wa miji na uendeshaji mbaya wa magari.

A traffic jam
Wahamasishaji wanasema kuwa kuendesha baiskeli na kutembea kunaweza kusaidia kupunguza msongamano katika baadhi ya miji barani Afrika huku ikisaidia nchi kupunguza uzalishaji wa hewa chafu za ukaa zinazoongeza joto sayarini. Picha:  AFP/Tony Karumba

Wataalam wanaamini kushughulikia maswala hayo ya usalama kunaweza kupelekea kuzuka usafari mazoezi barani kote, jambo ambalo litaleta manufaa mengi.

"Kutembea na kuendesha baiskeli kuna manufaa mengi kwa watu na kwa sayari, huboresha afya, hupunguza kiwango cha gesi ya ukaa tunachozalisha na kuboresha hewa," alisema Rob de Jong, mkuu wa kitengo cha usafiri cha UNEP.

 Ripoti ya UNEP iligundua kuwa mtu ambaye anaendesha baiskeli badala ya kufanya safari fupi tano kutumia gari kwa wiki hupunguza kiwango cha gesi ya ukaa anachozalisha kwa kilo 86 kwa mwaka.

Kuachana na magari na mabasi madogo, ambayo mengi yanaendelea kuzeeka na kuchafua mno, kutasaidia pia kupunguza aina nyingine za uchafuzi wa hewa, alisema de Jong.

"Mengi ya magari haya hutoa hewa chafu mara 10 ya kiwango yanachopaswa kutoa," alisema de Jong, na kuiongeza kuwa katika nchi nyingi za Afrika idadi ya magari huongezeka maradufu kwa kila muongo.  "Umiliki wa magari unaongezeka kwa kasi kwa hivyo hili ni jambo tunalohitaji kuzingatia kwa kina."

Barabara kwa watu

Nchini Ethiopia, Seble Samuel, mpiganiaji wa matumizi ya baiskeli, alianzisha kampeni inayojulikana kama Barabara Kuu kwa Matumizi ya Watu, ambayo, Jumapili ya mwisho ya kila mwezi, hushuhudia barabara kufungwa kwa magari.

Siku hizo, barabara huonekana kuwa na sherehe huku mamia ya waendesha baiskeli wakijumuika na watu wanaoteleza kwenye barafu, waendesha baiskeli, wakimbiaji wa mazoezi ya viungo na familia zinazojiburudisha na mandhari. 

Vuguvugu hili lilianzia Addis Ababa lakini sasa limeenea katika miji mingine nchini Ethiopia, kama vile Jimma Mekelle na Bahir Dar.

"Niliishi Amerika Kusini na kuona jinsi siku za barabara kwa matumizi ya watu yalivyounganisha jami" Samuel alisema. "Nchini Ethiopia, kuendesha baiskeli kunaonekana kama kitu kinachofanywa na watu maskini. Ikiwa tutaondoa vikwazo hivyo .... tunaweza kukabiliana na uchafuzi wa hewa huku tukikuza usafiri unaojali afya na endelevu.”   

Kwa masasisho ya hivi punde kuhusu Wiki ya Tabianchi barani Afrika, tembelea kuangazia ushughulikia wa mazingira na UNEP.

Mpango wa Afrika nzima wa Usafari Mazoezi

UNEP inaunga mkono Mpango wa Utekelezaji wa Afrika nzima wa Usafari Mazoezi, utakaoonyesha kujitolea kwa serikali kwa usafari mazoezi kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.  Juhudi hizo zinazinduliwa katika Kongamano la Kimataifa la Walk21 mjini Kigali, Rwanda, mwezi wa Oktoba.

Masuluhisho katika Sekta Sita kwa janga la mabadiliko ya tabianchi

UNEP iko mstari mbele kuunga mkono lengo la Mkataba wa Paris la kudhibiti kiwango cha joto duniani kisizidi nyuzijoto 2, na kulenga nyuzijoto 1.5, ikilinganishwa na viwango vya kabla ya viwanda.  Ili kufikia lengo hili, UNEP imeunda mwongozo wa Masuluhisho katika Sekta Sita, wa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu katika sekta mbalimbali kwa kuzingatia ahadi katika Mkataba wa Paris ili kuwezesha kuwa na mazingira thabiti. Sekta sita zilizoainishwa ni: nishati; viwanda; kilimo na chakula; misitu na matumizi ya ardhi; uchukuzi; na ujenzi na miji.