13 Dec 2019 Tukio Misitu

Kushirikisha jamii katika utunzaji wa misitu nchini Kenya

Photo by UN-REDD Programme

“Kila mara, ni vyema kutushirikisha, asema Kibarisho Leintoi, mama Mmasai mwenye umri wa miaka 36 aliye na watoto 8. “Hata kama sifahamu kusoma wala kuandika, ninafahamu kile familia yangu inahitaji ili kuishi: tunahitaji huduma ya matibabu na maji.” Maji ya unyunyuziaji wa shamba lake la nyanya na maji ya kondoo wake 5 na ng’ombe zake 5. Bila maji, mapato yake yatapungua. Hapo awali, alikuwa na uwezo wa kuwasomesha wawili kati ya wanawe; wengine iliwabidi kumsaidia nyumbani na kuchunga mifugo. Lakini baada ya mimea kutofanya vizuri kutokana na kiangazi, mmoja wa wanawe alilazimika kuacha shule baada ya kushindwa kumlipia karo.

image
Kibarisho katika shamba la mahindi. Picha na UN-REDD

Hapo awali, chemchemi ndogo ya maji ingetosha jamii nzima, bali kutokana na ongezeko la idadi ya watu na la mifugo, hali ni tofauti. Watu kutoka katika jamii ya Maji Moto iliyo karibu na kaunti ya Narok nchini Kenya, wanaelewa kuwa bwawa linaweza kuwasaidia kukusanya maji ili wayatumie kunyunyuzia mimea na kwa mifugo wao.

Jamii hiyo iliteua kamati ya watu saba, ikiwa ni pamoja na Kibarisho Leintoi. Kamati hiyo ilikutana na Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili ambao wamekuwa wakifanya kazi kusaidia jamii kubainisha mahitaji yao na kuyapa kipaumbele. Wakati jamii ya Maji Moto ilipoambia Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili kuwa walihitaji bwawa, walifundisha jamii hiyo jinsi ya kuandika pendekezo na kuwasaidia kupata mfadhili. Hela walizopata zilisimamiwa na jamii baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili ya jinsi kusimamia na kushughulikia pesa hizo.

image
Kibarisho na Noormejooli karibu na bwawa. Picha na UN-REDD

Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili walidhihirisha kuwa watu wa asili wana uwezo wa kumiliki na kutekeleza miradi iwapo watapata mafunzo mwafaka. Baada ya kufanya kazi na jamii kwa miaka mingi, Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili walishinda kandarasi ya Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa ya kutoa utaratibu wa kushirikisha wabia na kuandaa mwongozo wa jinsi ya kuwawezesha kutoa idhini yao bila kulazimishwa baada ya kuelimishwa. Hali hii itasaidia wafadhili na serikali kushirikisha jamii wanapoanzishisha miradi inayoathiri maisha yao.

“Ni muhimu kufahamu mtu wa kuongelesha katika jamii kwa sababu katika jamii ya wamaasai kwa mfano, kuna viongozi wa kitamaduni na viongozi vya utawala,” anasema James Twala, afisa wa mradi unaohusu mabadiliko ya tabianchi kwa Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili. “Katiba inasema kuwa iwapo miradi inaathiri maisha yao, wananchi ni sharti washirikishwe.”

Kwa kweli, katika mwaka wa 2010, taifa la kenya liliidhinisha katiba ambayo inathiri kwa kiwango kikubwa jinsi malighafi, ikijumuisha misitu, inavyosimamiwa. Usimamiaji wa malighafi hufanywa kwa ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na serikali katika ngazi ya kaunti. Katiba inataka wananchi washirikishwe katika kusimamia, kuhifadhi na kutunza misitu. Kwa hivyo, sheria mbalimbali kama vile Kifungu cha Sheria ya Usimamiaji na Utunzaji wa Misitu ya mwaka wa 2016 na Kifungu cha Sheria ya Mabadiliko ya Tabianchi cha mwaka wa 2016 vinalenga kuhusisha jamii za wenyeji na jamii za idadi ndogo ya watu katika usimamiaji na utunzaji wa mazingira. Pia zinapaswa kunufaika kutokana na mradi. “Hatubuni sheria mpya ila tunahakikisha kuwa watu wanafanya maamuzi wakiwa na uelewa bila kulazimishwa,” anaendelea Twala. “Hii ni kwa sababu iwapo miradi inaendeshwa na jamii, wanajamii wanahisi kuimiliki na hivyo kuna uwezekano mkubwa wa mradi husika kudumu kwa sababu kila mwanajamii binafsi na kwa jumla huwajibika na kushirikiana kutunza na kuuhifadhi hata mfadhili atakapoondoka.

image
James Twala akishauriana na mzee wa kijiji kutoka familia ya wamaasai. Picha na UN-REDD

Mwongozo ulioandaliwa na Wabia Wanaoboresha Maisha ya Watu wa Asili unahusisha mikutano ya mashauriano ambapo watu huelezea wanachohitaji na wanajamii kuelezwa kuhusu mradi husika, ikiwa ni pamoja na kiwango cha pesa zinazohitajika. Baada ya hapo, jamii huamua iwapo inakubali au la, na iwapo inakubali, viongozi wa jamii wanaweza kukubali kwa kuitikia tu au wakatia sahihi makubaliano. Makala ya makubaliano huonyesha kitakachojiri, mda utakaohitajika na matokeo. Mwishowe, jamii na shirika linahusika na utekelezaji wa mradi hufuatia jinsi mradi unavyotekelezwa.

The  Mradi wa UN-REDD umekuwa mstari wa mbele kuanzisha sera za ubunifu zinazothamini na kutunza misitu pamoja na huduma inazotoa kwa jamii na mifumo yake ya ekolojia. Kujitolea kutumia mbinu zinazojali haki za binadamu, kushirikisha wanajamii na wadau ni muhimu kwa malengo na kazi yake.  

 

Tangu mwaka wa 2017, Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ni mbia wa Chombo cha Ubia wa Kukabiliana na Hewa ya Ukaa katika Misitu, na kwa ushirikiano na Wizara ya Mazingira na Misitu walitumia mwongozo huu kuandaa pendekezo la mradi. Wakati wa mchakato huu, wadau walipendekeza kuwa sera ya misitu na sheria za Kenya zipitiwe upya ili kujumuisha matumizi ya mwongozo huu kama sehemu ya kujitolea kwa mchakato wa REDD+. Upitiaji huu mpya wa sera tayari umeanzishwa na unaendelea ili kuhakikisha idhini bila kushurutishwa ni sehemu ya sera za msitu nchini Kenya. “Inatoa fursa kwa jamii kushiriki katika mchakato wa kutoa maamuzi kuhusu miradi ya misitu ambayo wanategemea ili kuishi,” anasema Judy Ndichu, Mratibu wa Kiufundi wa Chombo cha Ubia wa Kukabiliana na Hewa ya Ukaa katika Misitu nchini Kenya.