Pixabay
12 Sep 2023 Toleo la habari Kutumia mazingira kushughulikia tabianchi

Saudia kuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2024 itakayoangazia uboreshaji wa ardhi, kuenea kwa majangwa na kustahimili ukame

Nairobi/Riyadh, Septemba 12, 2023 – Ufalme wa Saudia utakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2024 itakayoangazia uboreshaji wa ardhi, kuenea kwa majangwa na kustahimili ukame, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Saudia wametangaza leo.

Siku ya Mazingira Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, ilianzishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 1972. Kwa kipindi cha miongo mitano iliopita, siku hii imekua na kuwa mojawapo ya majukwaa makubwa zaidi duniani yanayohamasisha kuhusu masuala ya mazingira. Mamilioni ya watu hushiriki mtandaoni na kupitia shughuli za ana kwa ana, matukio na kuchukua hatua kote ulimwenguni.

Kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Majangwa, hadi asilimia 40 ya ardhi duniani imeharibika, na kuathiri moja kwa moja nusu ya idadi ya watu duniani na kutishia takriban nusu ya Pato la Taifa la kimataifa (Dola za Marekani trilioni 44). Idadi na muda wa ukame umeongezeka kwa asilimia 29 tangu mwaka wa 2000 - bila dharura, ukame unaweza kuathiri zaidi ya robo tatu ya jumla ya idadi ya watu duniani kufikia mwaka wa 2050.

Uboreshaji wa ardhi ni nguzo muhimu ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia (2021-2030), unatoa wito wa kutunza na kuboresha mifumo ya ekolojia kote ulimwenguni, ambayo ni muhimu ili kuweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Mwaka wa 2024 itakuwa maadhimisho ya miaka 30 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Majangwa. Kikao cha kumi na sita cha Kongamano la Nchi Wanachama (COP 16) wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Majangwa (UNCCD) kitafanyika katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh, kuanzia tarehe 2 hadi 13 Desemba  mwaka wa 2024.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Siku ya  Mazingira Duniani

Siku ya Mazingira Duniani ndicho chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa cha kuhamasisha duniani na kupelekea kuchukua hatua kwa manufaa ya mazingira. Siku inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1973, pia imekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha hatua za kufikia vipengele vya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Huku Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) likiwa mstari mbele, zaidi ya nchi 150 hushiriki kila mwaka. Mashirika makubwa, mashirika yasiyo ya kiserikali, jamii, serikali na watu mashuhuri kutoka kote ulimwenguni kupitisha chapa ya Siku ya Mazingira Duniani ili kutetea sababu za mazingira.

 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkubwa wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa