Pixabay
21 Sep 2023 Toleo la habari Kushughulikia kemikali na uchafuzi

Jamhuri ya Korea kuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 itakayoangazia kukomesha uchafuzi wa plastiki

Jamhuri ya Korea kuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 itakayoangazia kukomesha uchafuzi wa plastiki.

New York, Septemba 21, 2023 – Jamhuri ya Korea itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 itakayoangazia kukomesha uchafuzi wa plastiki kote ulimwenguni, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Jamhuri ya Korea walitangaza leo.

Siku ya Mazingira Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, ilianzishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 1972. Kwa kipindi cha miongo mitano iliopita, siku hii imekua na kuwa mojawapo ya majukwaa makubwa zaidi duniani yanayohamasisha kuhusu masuala ya mazingira. Mamilioni ya watu hushiriki mtandaoni na kupitia shughuli za ana kwa ana, matukio, hafla na kuchukua hatua kote ulimwenguni.

Dunia huzalisha zaidi ya tani milioni 430 za plastiki kila mwaka, thuluthi mbili ni vitu visivyodumu ambavyo hufanywa taka baada ya muda mchache, na kujaza bahari na, mara nyingi hujikuta katikamfmo wa chakula wa binadamu.

Katika mwaka wa 2024, Jamhuri ya Korea itakuwa mwenyeji wa Kikao cha Tano cha Kamati ya Majadiliano ya Serikali Mbalimbali kuhusu Uchafuzi wa Plastiki, ikijumuisha katika mazingira ya baharini. Mazungumzo hayo yanalenga kuunda chombo cha kisheria cha kimataifa kuhusu uchafuzi wa plastiki, kama ilivyoamrishwa na Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa kupitia azimio la 5/14.

"Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 utakuwa wakati muhimu wa uhifadhi wa mazingira kote ulimwengu kwani tunatarajia kuhitimisha makubaliano ya kimataifa ya plastiki.  Kama nchi mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025, Jamhuri ya Korea itaongoza juhudi za kimataifa za kuzuia uchafuzi wa plastiki," Waziri wa Mazingira wa Jamhuri ya Korea Han Wha-jin alisema. 

Kukomesha uchafuzi wa plastiki duniani ni mchango wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, ikiwa ni pamoja na kushughulikia mazingira, uzalishaji na matumizi ya bidhaa kwa njia endelevu, utunzaji wa bahari na kukarabati mifumo ya ekolojia na kuhifadhi bayoanuai.

"Ubia thabiti na ushirikiano imara ni uti wa mgongo wa ushirikiano wa mashirika ya biashara ya kimataifa, na UNEP inaishukuru Jamhuri ya Korea kwa kujitwika ukumu la kuandaa Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2025 katika harakati za kukomesha uchafuzi wa plastiki," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Siku ya  Mazingira Duniani

Siku ya Mazingira Duniani ndicho chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa cha kuhamasisha duniani na kupelekea kuchukua hatua kwa manufaa ya mazingira.  Siku inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1973, Siku hiyo pia imekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha hatua za kufikia vipengele vya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Huku Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) likiwa mstari mbele, zaidi ya nchi 150 hushiriki kila mwaka. Mashirika makubwa, mashirika yasiyo ya kiserikali, jamii, serikali na watu mashuhuri kutoka kote ulimwenguni hutumia fursa ya Siku ya Mazingira Duniani kutetea mambo yanayohusiana na mazingira.

Siku ya Mazingira Duniani iliandaliwa na Côte d'Ivoire – kwa msaada wa Uholanzi – katika mwaka wa 2023, nao Ufalme wa Saudia utandaa maadhimisho ya mwaka wa 2024.

 

Kuhusu Wizara ya Mazingira, Jamhuri ya Korea

Dhamira ya Wizara ya Mazingira ya Jamhuri ya Korea ni kuhifadhi mazingira asilia na maeneo ya makazi, kuzuia uchafuzi wa mazingira, kuhifadhi, kutumia na kukuza rasilimali za maji kwa njia endelevu.

 

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP)

UNEP ni mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira ulimwenguni. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano wa utunzaji wa mazingira kupitia kwa kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.  

 

Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:

Kitengo cha Habari na Vyombo vya Habari, Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa