06 Jul 2020 Tukio Majanga na mizozo

Visa vya COVID-19 vinavyotangazwa kila siku vinapoendelea kuongezeka, ripoti mpya inaelezea jinsi ya kuzuia ugonjwa mtandavu katika siku za ...

Photo by ILRI/HUPH/Ngan Tran

Mfumo anwai wa matibabu unaojali watu, wanyama, na mazingira ni muhimu ili kukomesha magonjwa kuenea kutoka wanyama hadi kwa binadamu.

Ebola, SARS, Zika, VVU/UKIMWI, homa ya West Nile na sasa COVID-19. Haya ni baadhi ya magonjwa sugu zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa iliyopita. Ijapokuwa yalitokea katika maeneo mbalimbali duniani, yanashabihana. Ni yale yanayoitwa "zoonotic" na wanasayansi yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu, na kwa wakati mwingine husababisha maradhi au vifo yanapotokea.

Sasa utafiti wa Kisayansi uliofanywa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mizigo (ILRI) unaonyesha kuwa iwapo nchi hazitachukua hatua madhubuti kukabiliana na magonjwa ambukizi yanayotoka kwa wanyama, mkurupuko wa magonjwa kama vile ya COVID-19 ni hali itakayotokea mara kwa mara.

"Watu hurejelea janga la homa ya mafua iliyotokea kati ya mwaka wa 1918 na 1919 na kudhani kuwa mkurupuko wa magonjwa ya aina hiyo hutokea tu mara moja kwa karne," anasema Maarten Kappelle, mkuu wa utafiti za kisayansi wa UNEP. "Lakini hayo si kweli kwa sasa. Tusiposhughulikiwa binadamu na mazingira kwa kiwango sawa, mikurupuko hii itaendelea kutokea mara kwa mara."

Utafiti huu, Kuzuia ugonjwa tandavu kutokea tena: Magonjwa yanayotoka kwa wanyama na jinsi ya kukabiliana nayo yasienee zaidi, ripoti iliyochapishwa tarehe 6 mwezi wa Julai, inaelezea jinsi ambavyo vijidudu 1,400 vinavyoeneza magonjwa kwa binadamu hutoka kwa wanyama.

Women working in the advanced animal health laboratories of ILRI, in Nairobi, Kenya (photo credit: ILRI/David White)
Wanawake wanaofanya kazi katika maabara ya kisasa ya ILRI yanayoshughulikia afya ya mifugo jijini Nairobi, nchini Kenya. Picha na ILRI/David White

Ijapokuwa magonjwa ambukizi kama vile COVID-19 yanazungumziwa mno na vyombo vya habari, magonjwa yaliyopuuzwa huua takribani watu milioni 2 kila mwaka, haswa kwa nchi zinazoendelea. Hiyo ni mara nne zaidi kuliko vifo kutokana na COVID-19 vilivyoripotiwa kwa sasa.

"Kwangu, magonjwa kutoka kwa wanyama, husababishwa na umaskini na kutokuwa na usawa," anasema Doreen Robinson, mwandishi mwenza wa ripoti hiyo na Mkuu wa Wanyapori wa UNEP. "Magonjwa haya huathiri watu zaidi katika nchi ambazo hazijaendelea sana. Kila mtu huanza kuyashughulikia tu pale ambapo majanga kama vile COVID-19 yanapotokea."

Magonjwa kutoka kwa wanyama yamekumba jamii tangu enzi za mawe na yalikuwa chanzo cha magonjwa mabaya tandavu kuwahi kutokea katika historia ikiwa ni pamoja na baa la mtoki lilitokea Enzi za Kati na ugonjwa tandavu wa homa ya mafua uliotokea mwanzoni mwa karne ya ishirini.

Lakini idadi ya watu inapokaribia bilioni 8, kufanya maendeleo kwa kasi kunafanya wanadamu na wanyama kuishi karibu, hali inayowezesha magonjwa kusambaa kwa urahisi kati ya spishi.

"Tunaponyakua maeneo zaidi, tunabuni fursa za kuwezesha usambasaji wake," anasema Eric Fèvre, profesa wamagonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama katika Chuo Kikuu cha Liverpool na aliyetuliwa pia kama mtafiti mwenza wa ILRI. "Kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia magonjwa tandavu mbaya zaidi na hatimaye, janga kama vile la  COVID-19, kadri shughuli zetu ainapoendelea kuongezeka."

Gharama ya kukabiliana na magonjwa kutoka kwa wanyama ni ghali. Mfuko wa Kimataifa wa Fedha unakisia kuwa  COVID-19 tu itasababisha kudidimia kwa uchumi kote duniani kwa asilimia 3 mwaka huu, na kupunguza uzalishaji kwa dola trilioni 9 kufikia mwaka wa 2021. Lakini hata miongo miwili kabla ya janga hili kutokea, Benki ya Dunia ilikadiria kuwa dola bilioni 100 hutumika moja kwa moja kugharamia magonjwa kutoka kwa wanyama.

Bashayider, a sheep farmer in Menz, Ethiopia (photo credit: Apollo Habtamu, ILRI).
Bashayider, mkulima wa kondoo eneo la Menz, nchini Ethiopia. Picha na Apollo Habtamu, ILRI

Ili kuzuia mikurupuko kutokea siku zijazo, nchi zinastahili kuweka mikakati iliyoratibiwa ya kisayansi ili kukabiliana na magonjwa kutoka kwa wanyama, anasema Delia Grace, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo aliye pia mtaalamu wa magonjwa ya wanyama katika shirika la ILRI na profesa wa usalama wa chakula katika Taasisi ya Mali Ghafi ya Uingereza. "Virusi havihitaji pasipoti ili kusafiri. Suala hili haliwezi kukabiliwa na nchi moja baada ya nyingine. Ili kufaulu kulishughulikia, ni sharti tuzingatie afya ya binadamu, afya ya wanyama na uboreshaji wa mifumo ya ikolojia."

UNEP na ILRI wanatoa wito kwa serikali ziweke mikakati zinazozingatia sekta mbalimbali na taaluma mbalimbali inayojulikana kama One Health. Inatoa wito kwa majimbo mbali na kutunza mifumo ya afya ya binadamu, yashughulikie masuala mengine kama vile - uharibifu wa mazingira na hitaji la ongezeko la ulaji wa nyama - hali inayorahisisha virusi kusambaa kati ya spishi. Hasa, inahimiza majimbo kukuza kilimo endelevu, kuimarisha viwango vya usalama wa chakula, kufuatilia na kuboresha masoko ya vyakula vya kiasili, kuwekeza kwenye teknolojia ili kufuatilia mikurupuko ya magonjwa, na kubuni nafasi mpya ya kazi kwa wale wanaoshiriki katika biashara ya wanyamapori.

Robinson pia anasema ni muhimu kwa serikali kuelewa vyema ni nini kinachosababisha magonjwa kutoka kwa wanyama. Hali hii inaweza kusaidia dunia kuzuia mengine mengine tandavu kama vile COVID-19.

"Kujitayarisha mapema na kuzuia hali tunayoshuhudia ya kufungwa kwa maeneo kote duniani—ni mojawapo ya manufaa ya kuwekeza kwenye utafiti kuhusiana na magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama," alisema. "Mikurupuko itatokea. Vijidudu vinavyosababisha magonjwa vitasafiri kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu, na hata kurudi tena kwa wanyama. Swali ni: Je, vitaenea umbali upi na vitasababisha madhara yepi?"

UKWELI KUHUSU MAGONJWA KUTOKA KWA WANYAMA

  • Magonjwa kutoka wa wanyama (yanayojulikana pia kama zoonoses) ni magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu na kutoka kwa binadamu hadi kwa wanyama.
  • Mifano ya magonjwa kutoka kwa wanyama ni VVU/UKIMWI, Ebola, Ugonjwa wa Lyme, ugonjwa wa malaria, kichaa cha mbwa na Homa ya West Nile bila kusahau ugonjwa unaosababishwa na virusi vipya vya korona wa COVID-19.
  • Baadhi ya wanyapori (ikijumuisha wanyama wagugunaji, popo, wala nyama na mamalia wa hali ya juu wasiokuwa wanadamu) wana uwezekano mkubwa wa kubeba vijidudu vinavyosababisha wangonjwa yanayotokana na wanyama, huku mifugo wakitumika kama nyenzo ya usambasaji kutoka kwa maeneo ya wanyapori hadi kwa binadamu wanaowafuga.
  • Katika nchi maskini zaidi duniani, magonjwa hatari yaliyopuuzwa yanayotokana hasa na mifugo, husababisha zaidi ya vifo vya binadamu milioni 2 kila mwaka.

 

Ili kujifahamisha zaidi, soma masuali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu magojwa kutoka kwa wanyama.

 

covid-19 response logo