23 Jun 2020 Tukio Misitu

Mjasiriamali mkenya akabiliana na ukataji wa miti kwa kutoa suluhu mpya ya nishati.

Ili kuadhimisha Siku ya Makampuni Ndogondogo Zaidi, Makampuni Ndogondogo na Makampuni Wastani ya Biashara, tunazungumza kuhusu wajasiriamali watano wanaosaidia kukabiliana na changamoto kuu za mazingira duniani.

Wakati ambapo Leroy Mwasaru alibaleghe, aligundua kuwa kuna tatizo kubwa katika shule ya bweni aliyosomea nchini Kenya. Mabomba yalipozeeka yalianza kuvuja na kupeleka maji taka ndani ya mito iliyokuwa karibu, mito ambayo ilitumiwa kusambaza maji kwa jamii zilizoishi karibu.

Leroy

Picha na Hivisasa

Mwasaru, mwenye umri wa miaka 22, alisema hangeweza kutulia alipoona hali hiyo ikiendelea. Kwa kusoma vitabu vya kiada, yeye na wanafunzi wenzake walianza kuunda mfumo unaoweza kutengeneza nishati kutoka kwa kinyesi cha mwanadamu. Sampuli kifani ya kwanza "ilifeli kabisa", anasema Mwasaru, lakini hatimaye kikosi hicho kiliunda kifaa kinachotumiwa kusambaza umeme shuleni humo.

Kufaulu huko kulimfanya Mwasaru kuanzisha kampuni ya Greenpact, kampuni mpya inayotengeneza mifumo ya kiwango cha juu kwa bei nafuu zinazojulikana kama vitengenezaji vya gesi asilia. Kazi hii inamfanya Mwasaru kuwa mjasiriamali mdogo mno kuainishwa kwenye orodha ya 'Forbes Africa' ya mwaka wa 2018 ya wajasiriamali 30 wenye umri wa chini ya miaka 30. 

"Lengo letu ni kuwa wazalishaji wakubwa mno wa nishati asilia barani Afrika," anasema Mwasaru, anayenuia kuwawezesha wakulima, taasisi na makaazi ya watoto kumiliki mfumo huo.

Mfumo wa Greenpact unatumiwa na wakenya 15,000. Mtambo wake unaounganishwa na mabomba ya taka majumbani, hukusanya taka na kwa usaidizi wa kemikali, huifanya kuwa gesi inayoweza kutumiwa kupika. Mfumo huu umaanisha kuwa wakenya hawahitaji kukata miti kupata kuni, sababu moja kuu ya ukataji wa miti msituni katika nchi ambayo tayari imeshapoteza zaidi ya theluthi moja ya maeneo ya bahari katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.

  "Watu hawa sasa wanaweza kupika bila kutumia kuni au makaa, ambavyo ni hatari kwa afya yao na kwa mazingira," anasema Mwasaru. "Kwa kutumia nishati jadidifu isiyochafua mazingira, tunapiga hatua za kuboresha mazingira. Na kila hatua ni muhimu."

Kazi ya Mwasaru ni mfano mzuri ya jinzi vijana wajasiriamali wanavyoweza kusaidia kukabiliana na changamoto kuu za mazingira, anasema Gabriel Labbate, msimamizi wa kikosi cha Programu ya Umoja wa Mataifa ya Kushirikiana Kupunguza Uzalishaji wa Gesi Chafu kutokana na Ukataji wa Miti na Uharibifu wa Misitu. Taasisi hii husaidia mno vuguvugu la REDD+, juhudi za kimataifa za kukabiliana na uharibifu wa misitu katika nchi zinazoendelea.

"Uhusiano na REDD+ ni dhahiri," anasema Labbate. "Mifumo inayozalisha nishati kutoka kwa taka husaidia kupunguza mojawapo ya sababu za ukataji wa miti kwa kuzalisha nishati ya kudumu, kupunguza sababu zinazopelekea ukataji wa miti, na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Kazi ya Mwasaru katika kampuni ya Greenpact imeathiriwa na COVID-19. Kwa sasa, anashirikiana na mamake ambaye ni mwanamtindo, kutengeneza barakoa za kutumiwa hospitalini na zahatini. Lakini pale ambapo janga hili litaisha, anataka kupanua biashara yake hadi kwenye mikahawa kwa kusaidia wauzaji wa chakula mijini kutumia taka kutoka kwa viumbe kuzalisha nishati.

"Sisi kama waafrika tunapaswa kutatua matatizo yetu wenyewe," anasema. "Na kwa kufanya hivi, nina matumaini kuwa nitaweza kushawishi vijana kuthamini mazingira yo na kuwaza kuhusu mbinu wanazoweza kutumia kuyalinda."