26 Nov 2019 Toleo la habari Mabadiliko ya tabia nchi

Uzalishaji wa gesi chafu kote ulimwenguni ni sharti upungue kwa asilimia 7.6 kila mwaka kwa muongo mmoja ujao ili kufikia lengo la Mkataba w...

  • Kutokana na ahadi zilizopo zinazotolewa kwa hiari, ongezeko la joto duniani litafikia nyuzijoto 3.2
  • Teknolojia na elimu kuhusiana na sera ipo ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, lakini ni sharti mabadiliko yaanze sasa
  • Nchi wanachama wa G20 huzalisha asilimia 78 ya gesi chafu duniani. Lakini, nchi 15 wanachama wa G20 hawajatoa ahadi ya ni lini watakomesha uzalishaji wa gesi chafu kabisa

 

Geneva, Novemba 26, 2019 –  Tunapokaribia mwaka jao, mataifa bado hayajaimarisha juhudi zao kuhusiana na ahadi zao kuhusu Mkataba wa Paris kuhusiana na Mazingira. Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inaonya kuwa uzalishaji wa gesi chafu kote duniani usipopungua kwa asilimia 7.6 kwa kila mwaka kati ya mwaka wa 2020 na mwaka wa 2030 dunia haitafaulu kufikia lengo la Mkataba wa Paris la nyuzijoto 1.5.

Ripoti inayotolewa kila mwaka na UNEP ya Hatua Zilizosalia Kupunguza Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu inaonyesha kuwa hata iwapo ahadi zote zilizotolewa kwa hiari chini ya Mkataba wa Paris zitatekelezwa, kiwango cha joto kinatarajiwa kuongezeka kwa nyuzijoto 3.2 na kusababisha madhara mbalimbali mabaya zaidi kwa mazingira. Juhudi za pamoja zinapaswa kuimarishwa zaidi ya mara tano zaidi ya juhudi zilizopo ili kufikia kiwango cha joto kinacholengwa cha nyuzijoto 1.5 katika kipindi cha muongo ujayo.

Mwaka wa 2020 ni muhimu katika kushughulikia mazingira, huku Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa umoja wa mataifa ukakaofanyika Glasgow ukilenga kuweka utaratibu utakaofuatwa siku zijazo kukabiliana na hali hiyo. Nchi zinatarajiwa kuimarisha zaidi juhudi zake

"Kwa miaka kumi, Ripoti ya Hatua Zilizosalia Kupunguza Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu imekuwa ikitoa onyo - na kwa miaka kumi, dunia imeongeza tu kuzalisha hewa chafu,” alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres. Hakujawahi kuwa na wakati mwafaka kuliko huu wa kusikiliza maoni ya wanasayansi. Kukosa kushughulikia onyo hizi na kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na uzalishaji wa hewa chafu ni ishara kuwa tutaendelea kushuhudia kiwango kikubwa na hatari cha ongezeko la joto, cha dhoruba na cha uchafuzi wa hewa.”

Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) limetoa onyo kuwa nyuzijoto zikipanda zaidi ya 1.5, kiwango cha madhara kwa mazingira kitaongezeka.

"Kushindwa kwetu kuchukua hatua kali za pamoja mapema ili kushughulikia mabadiliko ya tabianchi inamaanisha kuwa ni sharti tupunguze uzalishaji wa gesi chafu sasa- kwa zaidi ya asilimia 7 kila mwaka, iwapo tutapunguza kwa kiwango kilekile kwa kipindi cha muongo mmoja ujao," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Hii inamaanisha kuwa nchi haziwezi kusubiri hadi mwishoni mwa mwaka wa 2020, wakati wa kutoa ahadi mpya za kushughulikia mazingira, ndiposa juhudi ziimarishwe. Nchi – na kila mji, eneo, makampuni ya biashara na kila mtu binafsi –wanapaswa kuchukua hatua sasa.”

“Tunahitaji kufaulu haraka kupunguza uzalishaji wa hewa chafu zaidi iwezekanavyo katika mwaka wa 2020 ikifuatiwa na kuimarisha juhudi kupitia Michango Inayobainishwa na Taifa ili kuanza mageuzi makuu kwa uchumi na kwa jamii. Ni sharti tugharamie miaka ambayo tulipoteza,” aliongezea. Tusipofaulu kufanya hivyo hatutafaulu kufikia nyuzijoto 1.5 zinazolengwa kabla ya mwaka wa 2030.”

Nchi wanachama wa G20 huzalisha asilimia 78 ya hewa chafu duniani lakini ni nchi tano tu wanachama wa G20 ambazo zimetoa ahadi ya ni lini watakomesha uzalishaji wa gesi chafu kabisa.

Kwa malengo ya mda mfupi, nchi zilizoendelea ni sharti zipunguze uzalishaji wa gesi chafu kwa kasi kuliko nchi zinazoendelea, ili kuwe na haki na usawa. Hata hivyo, ni sharti nchi zote ziongeze juhudi ili kuwa na matokeo mazuri kwa jumla. Nchi zinazoendelea zinaweza kupata funzo kutokana na juhudi zilizofanikiwa kutoka kwa nchi zilizoendelea; zinaweza kushinda nchi hizo na kuamua kutumia kwa kasi teknolojia isiyochafua mazingira.

La msingi, ripoti inasema ni sharti kila taifa liongeze juhudi kupitia Michango Inayobainishwa na Taifa (NDCs), kwa sababu malengo ya Mkataba wa Paris yako wazi. Katika mwaka wa 2020 mataifa yanahitaji kuwa na sera na mikakati ya kuyatekeleza. Masuluhisho ya kufikia malengo ya Paris yapo, lakini hayatekelezwi kwa kasi inavyohitajika au kwa kiwango kikibwa kinachohitajika.

Kila mwaka, Ripoti ya Hatua Zilizosalia Kupunguza Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu huchunguza pengo la kiwango cha uzalishaji wa gesi kinachokusudiwa kufikiwa kufikia mwaka wa 2030 na viwango vinavyolenga kufia nyuzijoto 1.5  na  nyuzijoto 2  kwa mjibu wa Mkataba wa Paris. Ripoti inaonyesha kuwa uzalishaji wa gesi ya ukaa umeongezeka kwa asilimia 1.5 kwa kila mwaka kwa kipindi cha karne moja iliyopita. Uzalishaji wa gesi chafu katika mwaka wa 2018, ukijumuisha mabadiliko kwenye matumizi ya ardhi kama vile ukataji wa miti uliongezeka zaidi ya kufikia gigatani za kabonidioksidi 55.3.

Ili kudhibiti kiwango cha joto, uzalishaji wa hewa chafu kila mwaka kufia mwaka wa 2030 unapaswa kuwa gigatani 15 za kabonidioksidi ikiwa ni chini ya kiasi kilichopo cha NDCs kinacholenga kufia nyuzijoto 2; kiwango hicho kinapaswa kupungua kwa gigatani 32 ili kufikia nyuzijoto 1.5 zinazolengwa. Kwa kuzingatia kila mwaka, hii inamaanisha upunguzaji wa uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 7.6 kwa mwaka tangu mwaka wa 2020 hadi mwaka wa 2030 ili kufikia nyuzijoto 1.5 zinazolengwa na kwa asilimia 2.7 kwa mwaka ili kufikia nyuzijoto 2 zinazolengwa.

Ili kuweza kupunguza hewa chafu, kiwango cha kujitolea kwa NDSs kinapaswa kuongezeka angalau mara tano ili kufikia nyuzijoto 1.5 zinazolengwa na kuongezeka mara tatu ili kufikia nyuzijoto 2 zinazolengwa.

Kuna uwezekano wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi kuwa nyuzijoto 1.5, yasema ripoti hiyo. Manufaa zaidi ya kushughulikia mazingira yanaendelea kueleweka zaidi-kwa mfano kuwa na hewa safi na kuimarisha kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Serikali, miji, kampuni za biashara na wadau wameimarisha juhudi zao. Masuluhisho, shinikizo na nia ya kuzitimiza malengo inaongezeka.

Kama ifanyavyo kila mwaka, ripoti hiyo hulenga sekta teule na kufuatilia kwa karibu uwezo wake wa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu. Mwaka huu inaangazia mabadiliko katika matumizi ya nishati na uwezo wa kuitumia vitu kwa njia nzuri, hali inayoweza kusaidia kupunguza pengo kwenye uzalishaji wa hewa chafu.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

*Makala ambayo hayajaruhusiwa kuchapishwa yanaweza kufanyiwa marekebisho kabla ya kuchapishwa.

NUKUU ZAIDI

Niklas Höhne, Mwanzilishi mwenza wa Taasisi ya NewClimate Institute

"Mabadiliko yameanza polepole lakini yanaenea kwa kasi. Tunaona kuwa katika maeneo yote, kuna wahusika wanaochukua hatua za kipekee. Kwa mfano, malengo ya kutozalisha gesi chafu kamwe na malengo ya kutumia nishati jadidifu kwa asilimia 100 yanaenea kwa kasi. Pia, kampuni kubwa zilizodhania kuwa haiwezekani kutokuwa na uzalishaji wa hewa chafu kabisa, zimeanza kuweka juhudi. Kinachohitajika sasa ni kuwa na watu wanaweza kupigiwa mfano kote ulimwenguni kutokana na juhudi zao."

John Christensen, Mkurugenzi wa Ubia wa UNEP DTU Partnership

"Tukiangalia kwa kipindi cha miaka kumi ambacho tumekuwa tukiandaa Ripoti ya Hatua Zilizosalia Kupunguza Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu, ni jambo la kushangaza kuwa licha ya onyo nyingi zilizotolewa, uzalishaji wa gesi chafu duniani umeendelea kuongezeka na haonekani kupungua hivi karibuni.

Upunguzaji wa uzalishaji wa gesi chafu unaohitajika unaweza tu kufikiwa kwa kufanya mabadiliko katika sekta ya nishati. Habari njema ni kuwa kutokana unafuu wa upatikanaji wa umeme kutokana na upepo na jua, changamoto kuu iliopo ni jinsi ya kubuni na kuendeleza mifumo ta nguvu za umeme kwa njia mwafaka inayowafikia wengi."

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ndilo msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire, Mkuu wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP, +254722677747, [email protected]

Alejandro Laguna Lopez, Afisa wa Mawasiliano wa Eneo la Ulaya, UNEP, [email protected]