11 Dec 2019 Toleo la habari Nature Action

Kolombia itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani kuhusu bayoanuai

Madrid, Desemba 11, 2019 – Tunapoelekea mwaka muhimu wakati wa kufanya maamuzi muhimu kuhusu mazingira, Kolombia, Ujerumani na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) walitangaza leo kuwa Kolombia itakuwa mwenyeji wa Siku ya Mazingira Duniani katika mwaka wa 2020 kwa ushirikiano na Ujerumani na kuwa itahusu bayoanuai.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni. Ni siku ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha kuhusu masuala ya mazingira kote ulimwenguni. Miaka inapoendelea kusonga mbele, imeimarika na kuwa jukwaa kubwa la kimataifa ya kufikia umma na masuala ya mazingira na huadhimishwa na mamilioni ya watu kwa zaidi ya nchi 100.

Wakitoa tangazo hilo wakati wa Kongamano la Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi la Umoja wa Mataifa mjini Madrid, Uhispania, Ricardo Lozano, Waziri wa Mazingira na Maendeleo Endelevu kutoka Kolombia, Jochen Flasbarth, Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, na Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, walisisitiza kuwa kukiwepo na aina milioni moja ya mimea na wanyama walio hatarini kuangamia, hakujawahi kuwa na kipindi mwafaka cha kutilia maanani suala ya bayoanuai kuliko sasa.

Colombia to host WED 2020

"Tunahitaji udharura, kujitolea na kuchukua hatua katika mwaka wa 2020 ili kushughulikia majanga kwa mazingira; pia ni fursa ya kutumia suluhu zinazojali mazingira kukabiliana na tabianchi," alisema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP. "Kila mwaka, Siku ya Mazingira Duniani ni jukwaa kuu la kuhamasisha na kushawishi watu, jamii na serikali kutumia suluhu zinazojali mazingira kote ulimwenguni ili kuchukua hatua kuhusu changamoto kuu za mazingira zinazoikabili sayari. Tuna shukuru Kolombia na Ujerumani kwa kuwa mstari wa mbele kuongoza hizi juhudi.

Mwaka wa 2020 ni muhimu kwa mataifa kujitolea kutunza na kuimarisha bayoanuai, huku China ikiwa mwenyeji wa mkutano wa 15 wa Kongamano la Wanachama wa COP 15 kuhusu Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Uanuai wa Kibayolojia mjini Kunming. Mwaka ujao pia unatoa fursa ya kuelekea kuanzishwa kwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia (2021-2030), na nia ya kuboresha kwa kiwango kikubwa mifumo ya ekolojia iliyoharibiwa na kuharibiaa ili kukabiliana na janga kwa mazingira, kuhakikisha kuna chakula cha kutosha, kuimarisha usambasaji wa maji na wa bayoanuai.

"Katika taifa la Kolombia tutakabiliana na changamoto kuu katika mwaka wa 2020, ni ndio wanapaswa kuwa wenyeji wa mkutano wa tatu na wa mwisho wa kikundi cha OEWG [kikundi kinachofanya kazi bila vizingiti] kinachangalia mpango wa bayoanuai baada ya mwaka wa 2020 kabla ya COP nchini China. Katika nchi ya Kolombia, tunatarajia kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia makubaliano yatakayotuwezesha kusonga mbele na kujitolea zaidi wakati tutakapokutana kwa COP Uchina; tunakubaliana na Ujerumani kutusaidia katika juhudi hizi za kimataifa na tunatumai kuwa tutafaulu kufanya kazi pamoja," alisema Ricardo Lozano, Waziri wa Mazingira wa Kolombia,

Nchi inajulikana kama yenye "uanuai mwingi" na iliyo na takribani asilimia 10 ya bayoanuai duniani, Kolombia inashikilia nambari moja kutokana na aina nyingi ya ndege na mimea wa "okidi" na inashikilia nambari ya pili kutokana na mimea, vipepeo, samaki wa maji safi na wanyama waoweza kuishi majini na kwenye ardhi kavu. Taifa hilo lina maeneo mengi yaliyo na kiwango cha juu cha bayoanuai ya kibayolojia katika mifumo ya Andean, ikijumuisha kiwango kikubwa cha aina ya wanyama waopatikana tu katika eneo hilo. Pia sehemu ya misitu ya Amazon inapatikana eneo hilo na pia lina mifumo ya unyevunyevu katika eneo la kibayojiografia la Chocó.

 "Hakuna kipindi mwafaka cha kushirikiana kwa ajili ya sayari kuliko sasa," alisema Jochen Flasbarth, Waziri wa Mazingira wa Ujerumani "Kushughulikia mazingira na kutunza bayoanuai ni masuala muhimu. Tunahitaji kuunda sera za kuzuia kuangamiza aina ya mimea na wanyama. Ujerumani ina furaha ya kusaidia Kolombia na nchi zinginezo wanachama ili kuufanya mwaka wa 2020 kuwa mwazo wa kuchukua hatua kwa manufaa ya bayoanuai."

Kwa mjibu wa ripoti ya kipekee iliyotolewa mwaka huu na Jukwaa la Kuunda Sera za Sayansi kati ya Mataifa kuhusu Bayoanuai na Huduma za Mifumo ya Ikolojia (IPBES), miekeo ya sasa kuhusu bayoanuai na mifumo ya ekolojia inasemekana kuwa kizingiti kwa asilimia 80 kwa malengo yaliyotathminiwa ya Malengo ya Maendeleo Endelevu yanayohusiana na Umasikini, baa la njaa, afya, uzalishaji na matumizi kwa njia endelevu, maji, miji, tabianchi, bahari na ardhi.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

 

Siku ya Mazingira Duniani

Siku ya Mazingira Duniani ni jukwaa linalotumiwa na Umoja wa Mataifa kuhimiza uhamasishaji wa kimataifa kuhusu kuchukua hatua kwa manufaa ya mazingira. Siku inayoadhimishwa kila mwaka tangu mwaka wa 1974, imekuwa jukwaa muhimu la kuwezesha kuimarisha vipengele vya mazingira juu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Chini ya uongozi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya nchi 150 hushiriki kila mwaka. Mashirika makuu, mashirika yasiyokuwa ya serikali, jamii, serikali na watu maarufu kutoka pembe zote za dunia hutumia nembo ya Siku ya Mazingira Duniani kuhamasisha watu kuhusu masuala ya mazingira.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa

UNEP ni msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira. Hutoa uongozi na kuhimiza ushirikiano katika kutunza mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo. 

 

Kwa maelezo zaidi, wasiliana na:

Keishamaza Rukikaire, Msimamizi wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP, +254717080753, rukikaire@un.org