05 Nov 2019 Toleo la habari Kushughulikia Mazingira

Benki ya Biashara na Maendeleo na UNEP washirikiana kufadhili tabianchi

Benki ya Biashara na Maendeleo na UNEP washirikiana kufadhili tabianchiirobi, Novemba 5, 2019  Wakitoa ahadi ya kuimarisha hatua zao za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Benki ya Biashara na Maendeleo(TDB) ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, leo walitia sahihi Mkataba wa Makubaliano na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Mkataba huo unaweka wazi mfumo wa ushirikiano utakaotumiwa na taasisi hizo mbili kufanya kazi kwa sekta mbalimbali muhimu ili kuyafikia malengo ya kimataifa kuhusiana na mazingira.

Katika sekta ya ufadhili wa nishati isiyochafua mazingira, TDB na UNEP watafanya kazi  kuimarisha uwekezaji utakaowezesha kufadhili sekta za kibinafsi na za umma ili kuziwezesha kusambaza teknolojia inayotumia nishati isiyochafua mazingira. Hii ni pamoja na kusaidia miradi changa ya maendeleo na kufadhili miradi ya nishati jadidifu. Pia, wameweka utaratibu wa kutoa fedha zitakowezesha kununua vifaa vinavyotumia nishati kidogo na  visivyotumia umeme mwingi ili kutumiwa majumbani na katika majengo ya biashara.

Kwa kuongezea, taasisi hizo mbili zitashirikiana kusaidia nchi wanachama wa TDB kupokea ufadhili kutoka kwa mfuko wa Green Climate Fund ili kuziwezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.

"Kama mwanachama wa Klabu ya Fedha za Maendeleo ya Kimataifa, kikosi kikuu  kinachofadhili miradi ya kimataifa ya maendeleo ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na ufadhili wa miradi ya mazingira, TDB inashirikiana na wabia wake kutekeleza  Ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu pamoja na yale ya Mkataba wa Paris kuhusu Mazingira. Kwa kushirikiana na wabia wa kimataifa kama UNEP, tunatarajia kutimiza ahadi za kimataifa za kusaidia Afrika kuimarika na kuwa na maendeleo endelevu," alisema Admassu Tadesse, Rais na Afisa Mkuu Mtendaji wa TDB.

Michael Awori, Afisa Mkuu wa Oparesheni wa TDB, aliongeza kuwa "kujitolea kwetu ni dhahiri kutokana na matumizi ya asilimia 70 ya nishati jadidifu katika sekta yetu ya kawi. Kwa kuzingatia rekodi tuliyoweka, sisi ni wabia mwafaka wa kushirikiana nao kufadhili miradi ya kudumu inayoleta maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali."

"Ijapokuwa  chumi za maeneo ya Afrika Mashariki na  ya Kusini mwa Afrika zinaendelea kuimarika, kuna uwezekano mkubwa wa kutumia nishati isiyochafua mazingira katika maeneo hayo. UNEP na TDB wanashirikiana kusaidia kuwepo na usambazaji mkubwa wa teknolojia isiyochafua mazingira na kutafuta rasilimali za kifedha zinazohitajika kukabiliana na changamoto za Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka wa 2030 ," alisema Joyce Msuya, Naibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP.

 

MAKALA KWA WAHARIRI

Kuhusu Benki ya Biashara na Maendeleo ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika
 Benki ya Biashara na Maendeleo ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika(TDB) iliyoanzishwa mwaka wa 1985,  ni taasisi ya kimataifa ilianzishwa kutokana na mkataba wa taasisi za kifedha za maendeleo. Ina mali ya thamani ya dola za Marekani bilioni 6. Lengo la benki hiyo ni kufadhili na kukuza biashara, kukuza uchumi kwenye ukanda na kuwezesha maendeleo endelevu kupitia kufadhili biashara, kufadhili miradi na miundo misingi, utunzaji wa mali na utoaji wa ushauri. Benki  hiyo hufanya kazi yake kwa njia inayowezesha kuleta maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na na kupunguza madhara kwa mazingira na kukuza matumizi ya nishati isiyochafua mazingira-ili kutimiza malengo ya Mkataba wa Paris na Malengo ya Maendeleo Endelecu (SDG) yanayohusiana na utunzaji wa mazingira. Kufikia sasa, asilimia 70 ya nishati inayotumiwa na benki ya TDB ni nishati jadidifu na kwa njia moja au nyingine, huchangia kwa SDGs.

Kuhusu Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ndilo msemaji mkubwa wa kimataifa kuhusu mazingira. Hubuni ajenda zinazohusiana na mazingira, huwezesha utekelezaji wa vipengele vya mazingira vinavyohusiana na maendeleo endelevu katika taasisi za Umoja wa Mataifa na kufanya kazi kama mhamasishaji mkuu wa masuala ya mazingira duniani. Lengo la UNEP ni kutoa uongozi na kuhimiza ubia katika utunzaji wa mazingira kupitia kuvutia, kuelimisha na kuwezesha mataifa na watu kuimarisha maisha yao bila kuhatarisha yale ya vizazi vijavyo.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Anne-Marie Iskandar, Afisa Mkuu wa Mawasiliano, Benki ya Biashara na Maendeleo
Keishamaza Rukikaire, Mkuu wa Habari na Vyombo vya Habari, UNEP